Jumapili, 28 Januari 2018

Kilimo cha nyanya

JUtangulizi:
• Nyanya ni zao la mboga ambalo hulimwa sehemu nyingi duniani kwa
ajili ya matumizi ya nyumbani na pia kama zao la biashara. Inahisiwa
kuwa asili ya nyanya ni nchi ya Peru/Equador huko Amerika ya Kusini.
Mmea huu ulianza kuzalishwa kama zao katika nchi ya Mexico na
baadaye kusambaa katika nchi nyingine za ulimwengu.

Uzalishaji wa nyanya duniani na hapa Tanzania
Nchi zinazolima nyanya kwa wingi duniani ni pamoja na USA, Italia na
Mexico. Kwa upande wa Africa nchi zinazo lima ni kama; Malawi,
Zambia na Botswana.
Zao hili hulimwa pia katika nchi za Africa Mashariki, ikiwemo Kenya,
uganda na Tanzania.
Zao la nyanya linalimwa karibu maeneo yote ya Tanzania. Uzalishaji
wa nyanya ni mkubwa kuliko mazao mengine ya mbogamboga
yanayolimwa hapa Tanzania, uzalishaji wa nyanya kwa mwaka ni
jumla ya tani 129,578 ikiwakilisha asalimia 51 ya mazao yote ya
mboga. Kwa mujibu wa Wizara ya kilimo ya Tanzania maeneo
yanalolima sana nyanya ni pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro (Hai, Moshi
na Rombo), Arusha (Arumeru), Morogoro (Mgeta), Tanga (Lushoto),
Mbeya (Mbeya vijijini) na Singida. Morogoro ndiyo inayoongoza kwa
kilimo hichi ikiwa na wazalishaji wenye zaidi ya hekta 6,159 (ekari
15,398). Pamoja na kwamba eneo la uzalishaji linaongezeka kwenye
maeneo mengi lakini uzalishaji wa nyanya bado ni mdogo sana.
Uzalishaji mdogo unasababishwa na kupungua kwa rutuba ya ardhi,
upepo, joto, ukame. Sababu nyingine ni pamoja na ukosefu wa aina za
nyanya zenye mavuno mengi amabazo zinahimili mazingira ya kwetu,
wadudu, magonjwa na magugu.
Mazingira
• Hali ya Hewa:
Nyanya hustawi vizuri zaidi kwenye mazingira ya joto la wastani
kuanzia nyuzi joto 18-27 sentigreti. Mvua nyingi husababisha mlipuko
wa magonjwa ya ukungu kama vile Baka jani chelewa n.k.)
• Udongo:
Nyanya hustawi kwenye aina zote za udongo kuanzia udongo wa
kichanga, mweupe wa tifutifu hadi udongo wa mfinyanzi, ili mradi uwe
na mboji ya kutosha na usiosimamisha/tuamisha maji. Pia uwe na
uchachu wa wastani yaani pH 6.0 – 7.0.
Aina za Nyanya
Kutokana na tabia ya ukuaji, nyanya zinagawanyika katika makundi
mawili:
1. Aina ndefu ( intermediate) kwa mfano ANNA F1, Tebgeru 97. Aina
hizi hufanya vizuri zaidi zinapopandwa ndani ya greenhouse. Uvunaji
wake ni wa muda mrefu, zipo ambazo zinavunwa hata zaidi ya miezi 6,
yaani hiyo miezi 6 ni ya uvunaji.
2. Aina fupi (determinate) kwa mfano Tanya, Cal J, Mwanga, Onyx,
Roma VF (nyanya mshumaa)
Kotokana na uchavushaji, nyanya zinagawanyika makundi mawaili:
1. OPV (Open Pollinated Variety) – Aina za kawaida
2. Hybrid – Chotara: Hizi ni aina zenye mavuno mengi, kati ya hizo
zipo aina fupi na ndefu.
Katika karne hii ya 21, nyanya zinazopendelewa kulimwa zaidi na
wakulima, ni zile zinazoweza kuvumilia magonjwa, zinazo zaa sana, na
zenye ganda gumu ili kufanikisha usafirishaji, na kuhifadhika kwa siku
nyingi bila kuharibika mapema.
Kwenye Kilimo – 2
Kuandaa Kitalu cha Nyanya
Mambo muhimu ya kuzingatia:
• Kitalu kiwe karibu na maji ya kutosha na ya kudumu
• Kiwe sehemu iliyowazi na yenye udongo ulio na rutuba ya kutosha
• Eneo la kitalu kama ni kubwa liwe tambarare au na mwiinuko kidogo
ili kuepuka maji yasituame kwenye kitalu, mtelemko ukiwa mkali sana
nao sio mzuri kwani husababisha mmomonyoko wa udongo.
• Kitalu kiwe sehemu ambayo haikuwa na zao la nyanya au viazi
mviringo (au mazao ya jamii ya nyanya k.m. mnavu, biringanya n.k.)
• Kiwe sehemu ambayo ni rahisi kupata huduma zote muhimu kwa
urahisi, ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa miche kwenda sehemu
nyingine. Pia kurahisisha usambazaji wa miche kwenda sehemu
nyingine.
Kuandaa Matuta ya Kusia Mbegu za Nyanya
Aina ya matuta:
– matuta ya makingo (sunken seed bed)
– matuta ya kunyanyulia udongo (raised seed bed)
– matuta ya kawaida (flat seed beds)
Mambo Muhimu ya Kuzingatia wakati wa Kuandaa Matuta
• Tuta liwe na upana kati ya sentimita 90-120, na urefu wowote, [ili
mradi muhudumu anaweza kutoa huduma nyingine zote kitaluni bila
kukanyaga miche].
• Kwatua/lima kina kirefu cha kutosha kiasi cha sentimita 15-20 ili
mizizi iweze kusambaa vizuri ardhini.
• Choma takataka juu ya kitalu, au funika tuta kwa nailoni, majuma 4-8
ili kuua vimelea vya magonjwa na wadudu.
• Wakati wa kuandaa, kitalu, ongeza mbolea aina ya samadi/vunde au
mboji kwenye udongo kisha kwatua ili ichanganyike vizuri na udongo.
• Changanya kiasi cha debe 1 hadi 2 kila baada ya mita moja (hatua
moja) mraba.
• Tuta lisiwe na mabonde mabonde au mawe mawe ambayo yanaweza
kuzuia usambaaji mzuri wa mbegu kwenye tuta, lisawazishwe vizuri ili
kuhakikisha usambazaji mzuri wa mbegu na kuepuka mbegu kufukiwa
chini mno kiasi ambacho hazitaota.
Faida na Hasara za Matuta yaliyotajwa hapo juu
1. Matuta ya kunyanyulia udongo (raised seed beds);
– matuta ya namna hii huruhusu maji, hewa na mizizi kupenya kwenye
udongo kwa urahisi zaidi.
– Mazao ya mizizi hupata nafasi ya kutosha kutanuka haraka zaidi
– Matuta haya hayatuamishi maji kama mengine, hivyo hutumika zaidi
kwenye maeneo yanayokuwa na mvua mara kwa mara.
Hasara:
o Matuta ya namna hii yana sababisha sana mmomonyoko wa udongo
kama hayakutengenezwa vizuri.
2. Matuta ya makingo (sunken seed beds):
Faida:
· matuta haya ni rahisi kutengeneza
· hutumika wakati wa kiangazi ili kuhifadhi maji na unyevu
· nyevu mdogo unaopatikana ardhini
· ni rahisi kumwagilia kwa kutumia maji ya mfereji au bomba
· huhifadhi unyevu nyevu kwenye ardhi kwa muda mrefu
· huzuia mmomonyoka wa ardhi
Hasara:
· Matuta ya aina hii hayawezi kutumika kwenye maeneo yenye
· mvua nyingi.
3. Matuta ya kawaida (flat seed beds):
Faida:
· ni rahisi sana kutengeneza kwani udongo ukisha kwatuliwa
· na kusambazwa mbegu huoteshwa
· ni rahisi kutumia eneo kubwa kuotesha mbegu
Hasara:
Matuta ya aina hii hayawezi kutumika kwenye maeneo yenye mvua
nyingi.
Kusia Mbegu
• Hakikisha ubora na uotaji wa mbegu kabla ya kuzipanda kitaluni
(germination test)
• Weka mistari kwenye tuta kulingana na ukubwa wa tuta, lakini
mistari isiwe chini au zaidi ya sentimita 15-20 toka mstari hadi mstari
• Kina cha mistari kisiwe cha kutisha bali kiwe kati ya sentimita 1-2
• Matuta yapate maji ya kutosha siku moja kabla ya kusia mbegu. Ni
vizuri kutumia chombo cha kumwagilia (watering can).
• Mbegu ziatikwe kwenye mistari na zisambazwe vizuri ili kufanikisha
usambaaji mzuri wa mbegu kwenye tuta. Changanya mchanga laini na
mbegu kisha sambaza kwenye mistari iliyoandaliwa kwenye tuta.
Mbegu zinaweza pia kuatikwa kwenye tuta bila mistari, lakini
zisambazwe kwa uwiano mzuri kwenye tuta ili kupunguza
msongamano. Msongamano husabisha magonjwa ya fangasi kama vile
kinyausi (damping off) au ukungu (blight).
• Weka matandazo kiasi cha kutosha ambacho hakitazuia kuota kwa
mbegu.
• Mara baada ya kuatika mbegu, mwagilia maji kiasi cha kutosha
kulingana na unyevu nyevu ulioko ardhini
Mambo ya Kuzingatia baada ya kusia mbegu pamoja na Matunzo
Kitaluni
• Mwagilia maji kwenye kitalu baada ya kuotesha kulingana na unyevu
nyevu uliopo kwenye udongo.
• Miche yote ikisha ota, ondoa matandazo, kisha weka chanja ili
kupunguza mionzi ya jua ambayo inaweza kuunguza miche michanga.
(kipindi cha baridi si muhimu sana)
• Punguzia miche (thinning) ili ibakie kwenye nafasi ya kutosha. Hivyo
miche ibakie kwenye umbali wa sentimita 2.5 – 4. Hii itapunguza
magonjwa ya ulemavu na mnyauko, pia itasaidia kupata miche bora na
yenye nguvu.
• Endelea kumwagilia hadi miche ifikie kimo kinachofaa kuhamishia
shambani.
• Punguza kiwango cha umwagiliaji maji, siku chache kabla ya
kuhamishia miche shambani, yaani siku 7-10.
Kanuni na Mbinu za kuhamisha miche toka Kitaluni kwenda shambani
(Transplanting
Rules)
• Mwagilia miche masaa machache kabla ya kuhamishia miche
shambani ili wakati wa kung’oa miche mizizi ishikamane vizuri na
udongo.
• Kabla ya kuhamisha miche, mashimo yawe yamekwisha andaliwa
katika nafasi zinazo stahili huko shambani.
• Miche ihamishwe wakati wa jioni ili kuepuka madhara yanayoweza
kusababishwa na jua.
• Kwa ujumla karibu mazao yote ya mboga mboga huwa tayari
kuhamishiwa shambani yakiwa na majani kamili kati ya 2-6 pamoja na
mizizi mingi iliyostawi vizuri.
• Mche lazima uwe na afya nzuri, uwe umenyooka vizuri, hivyo miche
yote iliyonyongea au myembamba kupita kiasi isichukuliwe wakati wa
kupeleka shambani.
• Ng’oa miche kwa uangalifu hasa pamoja na udongo wake kwa
kutumia vifaa husika ili mizizi isidhurike.
• Miche ihamishiwe shambani mapema mara baada ya kung’olewa
toka kitaluni.
• Wakati wa kuhamisha miche, uangalifu mkubwa utumike ili
kutoharibu miche/mizizi.
Maandalizi ya Shamba la Nyanya
• Shamba la nyanya liandaliwe mwezi 1-2 kabla ya kupanda miche.
• Mara baada ya kulima choma nyasi juu ya udongo au ondoa magugu
yote yanayoweza kuhifadhi wadudu na magonjwa ya nyanya.
• Siku moja au mbili kabla ya kuhamishia nyanya shambani, mwagilia
sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuhamishia nyanya.
• Nafasi kati ya mche hadi mche ni wastani wa sentimita (50-60) x
(50-75) kutegemeana na aina au hali ya hewa. Kama ni kipindi cha
baridi ni vyema nyanya zikapandwa mbalimbali ili kuruhusu
mzungungo wa hewa na kuzuia magonjwa ya fangasi.
Jinsi ya kupanda miche:
• Hamisha miche toka kitaluni pamoja na udongo wake
• Sambaza mizizi vizuri kwenye shimo bila kukunja.
• Fukia miche kina kile kile ambacho shina lilikuwa limefukiwa
bustanini.
• Mwagilia maji ya kutosha kulingana na unyevunyevu uliopo kwenye
udongo kasha weka matandazo na kivuli ili kupunguza uharibifu
unaosababishwa na mionzi ya jua.
Mambo muhimu ya kuzingatia baada ya kuhamishia Miche Shambani
• Kagua shamba mara kwa mara ili kujua maendeleo au matatizo
yaliyoko shambani mapema
• Hakikisha shamba ni safi wakati wote, palilia shamba na hakikisha
magugu yote hasa yale ya jamii ya nyanya yamelimiwa chini.
• Ondoa mimea iliyoshambuliwa na magonjwa au ondoa sehemu
zilizoshambuliwa, kisha zifukiwe chini au kuunguza moto.
• Punguza matawi na vikonyo ili kuongeza mwanga wa kutosha
kwenye nyanya pamoja na kuruhusu mzunguko wa kutosha wa upepo
na kusababisha mazingira magumu ya wadudu maadui kwenye nyanya,
hasa wale wanaopenda kiza na magonjwa yanayopendelea
unyevunyevu.
Asante sana:
Kwa leo tutaishia hapa, kwenye makala zifuatazo tutajikita kuchambua
baadhi ya wadudu wasumbufu kwa nyanya, tutaangalia pia masoko ya
nyanya pamoja na teknolojia mbalimbali za uzalishaji pamoja na
usindikaji.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

UFUGAJI WA KUKU KIBIASHARA

JIFUNZE KUFUGA KIBIASHARA HASA KWA WAFUGAJI WA KUKU KWA YOYOTE ATAKAYE HITAJI TEMPLATE HII NA ZINGINE ANITAFUTE KWENYE NO 0756841313